NEC YATOA UHURU KWA VYOMBO VYA HABARI SIKU YA UCHAGUZI


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) itaruhusu waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali kufika kwenye vituo vya kupigia kura na kufanya mahojiano na wapiga kura pamoja na wasimamizi wa uchaguzi kuhusu zoezi la kupiga kura litakavyokuwa likiendelea.


Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima wakati wa mafunzo ya siku mbili ya waratibu wa uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo na wilaya na maafisa wa uchaguzi yaliyofanyika mjini Morogoro.


Mkurugenzi huyo amesema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwani kwa mara ya kwanza waandishi wa habari wataruhusiwa kufika katika vituo vya uchaguzi kwa lengo la kupata habari kutoka kwa wasimamizi wa uchuguzi na hata wapiga kura kuhusu namna uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 utakavyokuwa ukiendelea.


Hata hivyo Kailima amesema kuwa kwa sasa tume inaandaa mwongozo utakaoeleza taratibu na mipaka ya waandishi wa habari pamoja na watakaohusika kutoa habari katika vituo hivyo vya kupigia kura.


Katika hatua nyingine Kailima amesema kuwa NEC imepata taarifa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) iliyotabiri kuwa mwezi Oktoba kutakuwa na mvua hivyo NEC imejiandaa kukabiliana na changamoto hiyo.


Hivyo amewataka wasimamizi wa uchaguzi kubaini mapema maeneo ambayo yanaweza kuingia maji na kuweka tahadhari ili kuepuka usumbufu kwa wapigakura ama uharibifu wa vifaa vya kupigia kura zikiwemo karatasi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527