Kufuatia
hofu iliyotanda ya baadhi ya wagombea
kukatwa majaina yao Chama Cha mapinduzi Mkoani Shinyanga kimewatoa hofu
wanachama wake kwamba hakutakuwa na utaratibu wa kuwakata baadhi ya
majina wagombea wa ngazi ya udiwani na wabunge katika kipindi cha
uchaguzi mkuu ujao utakao fanyika mwezi Oktoba 2015.
Kauli
hiyo imetolewa juzi na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja wakati
akizungumza kwenye sherehe za ushindi wa serikali za mitaa 2014
zilizofanyika katika kijiji cha Nyandekwa kata ya Nyandekwa wilayani
Kahama na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama wilaya na mkoa.
Mgeja
alisema CCM mkoa wa Shinyanga haina agenda ya kukata jina la mgombea atakayekubalika
kwa wananchi na kwamba maneno yanayozushwa
na baadhi ya wanachama mbalimbali yana lengo la kupotosha wanachama na wananchi.
“Haya
maneno yanayozushwa yana lengo la kuwakatisha tamaa baadhi ya wanachama wenye
nia ya kugombea nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka
huu 2015,naombeni muwapuuze”,alisema Mgeja.
Mgeja
alisema CCM itatenda haki kwa kila mwanachama atakayegombea nafasi yeyote
ndani ya chama na kuongeza kuwa suala la mwanachama la kuchaguliwa ama
kutochaguliwa ni suala la wanachama ndiyo watakaoamua kupitia mikutano halali
ya chama.
Aidha
aliwatahadharisha viongozi wa CCM mkoani Shinyanga humo wasiwachagulie wagombea
wanachama na wananchi kwani kufanya hivyo ni sawa na kutengeneza bomu ambalo linaweza
kulipuka Oktoba 2015 na hakuna mtu au kiongozi yeyote ndani ya chama atayeweza
kulizima.
Katika
hatua nyingine Mgeja alitoa onyo kali kwa baadhi ya wanachama wenye nia ya
kugombea ambao wameanza kupita pita kwenye majimbo na kata kwa kutumia
jina la “Ikulu” kuwa wametumwa na Ikulu kwa lengo la kuungwa mkono hali ambayo
aliikemea vikali na kuagiza viongozi ngazi za Wilaya na kata kufuatilia nyendo
zao na kuwataka kuacha tabia hiyo mara moja.
Aidha
alitoa angalizo kwa wagombea wenye nia ya kusubiria kubebwa au kupakatwa na
wakubwa kwani kwa uchaguzi wa sasa hauna nafasi kwa watu kama hao bali watu hao
watajiuza wenyewe ndani na nje ya chama kwa historia ya utendaji wao wa kazi
ambao ndiyo utakaowabeba.
“Nitoe
angalizo kwa wale wote wenye nia ya kusubiri kubebwa na ama kupakatwa na
wakubwa niwambie tu uchaguzi huu wa sasa hauna nafasi kwa watu kama hao bali
watajitangaza na kujiuza wenyewe kwa historia ya utendaji wao wakazi ambao ndiyo
utakao wabeba”,aliongeza Mgeja.
Hata
hivyo Mgeja aliwapongeza viongozi na wanaCCM wa kata ya Nyandekwa wilayani Kahama kwa
ushindi wa asilimia mia moja katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuongeza
kuwa ushindi huo wa kishindo umetokana na viongozi kuteua wagombea wazuri
waliokubalika kwa wananchi.
Kata
hiyo ya Nyandekwa yenye vijiji saba ambavyo ni Nyandekwa,Chalya,Lowa,Kakebe,Kalengwe,Kigungumuli
na Baduha ambapo katika uchaguzi wa serikali za mitaa Chama Cha Mapinduzi
kilishinda viti vyote kwa asilimia 100 na hivyo kupelekea kata hiyo
kuandaa sherehe za ushindi ambapo mgeni rasmi katika sherehe hiyo alikuwa ni
mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja.
Na Kadama Malunde-Kahama