DIWANI WA CHADEMA AMTEMBEZEA KICHAPO CHA MAANA MAMA MJAMZITO

 http://mtanzania.co.tz/wp-content/uploads/2015/02/Diwani.jpg

Diwani wa Kata ya Saranga wilayani Kinondoni, Ephraim Kinyafu (CHADEMA) anadaiwa kumshambulia kwa mateke na fimbo, Aisha Mosses, ambaye ni mjamzito akimtuhumu kuwa ni mamluki.

Tukio hilo lilitokea jana katika Mtaa wa Saranga ambako hatua ya uandikishaji wananchi kwa ajili ya kurudia uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao awali ulivurugika, lilikuwa likiendelea.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa mtaa huo, Majaliwa Kayombo alisema tukio hilo lilitokea mchana.

“Wananchi walikuwa wakija kujiandikisha kwa ajili ya kurudia uchaguzi kutokana na ule wa awali kuvurugika… Aisha wakati huo alikuwa amekaa chini akipumzika, Kinyafu akiwa na vijana walimvamia na kumshambulia,” alisema Kayombo.

Kayombo alisema mama huyo alipigwa kwenye kiwiko cha mkono na begani.

“Ingawa tulijitahidi kuwadhibiti na kuwasihi kuacha kumpiga mama huyo lakini waliendelea na mwishowe wakakimbia, tulimchukua na kwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuph,” alisema.

Alisema Aisha alipatiwa fomu ya matibabu ya PF3 na kwenda kutibiwa katika zahanati ya Mbezi Mwisho pamoja na oda ya kuwatafuta watuhumiwa (RB).

Hata hivyo Kinyaf alipotafutwa ili kupata ufafanuzi kuhusiana na tuhuma hizo lakini alisema hana taarifa juu ya tukio hilo.

“Ndiyo mwandishi…. nimekusikia lakini binafsi sina taarifa juu ya tukio hilo unalonieleza labda nifuatilie zaidi,” alisema kabla ya kukata simu yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura alisema taarifa hizo bado hazijamfikia na kuahidi kuzifuatilia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527