RAIS KIKWETE ATEMA MAWAZIRI 60, MAWAZIRI 16 TU WANUSURIKA!!

Panga pangua ya saba ya Baraza la Mawaziri iliyofanyika juzi imefikisha mawaziri 61 waliotemwa, kujiuzulu au kufariki dunia tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, huku mawaziri 16 wakihimili mawimbi hayo hadi sasa.

Katika mabadiliko hayo saba yaliyofanywa katika kipindi cha miaka tisa, wako waliobadilishwa wizara, kupandishwa kutoka naibu waziri kuwa waziri kamili, huku sura mpya zikiingizwa.

Mabadiliko hayo yalitokana na mawaziri kutakiwa kuwajibika kutokana na kashfa mbalimbali, huku mengine yakitokana mawaziri kufariki na moja likitokana na Waziri Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katika panga pangua hiyo, mawaziri 16 wamefanikiwa kudumu katika baraza hilo tangu Rais Kikwete aingie madarakani ambao ni Sofia Simba, Profesa Mark Mwandosya, Stephen Wasira, Dk Hussein Mwinyi na Dk John Magufuli.

Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe, Dk Shukuru Kawambwa, Hawa Ghasia, Dk Mary Nagu na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, alikuwa naibu waziri na baadaye waziri wa Tamisemi.

Mawaziri wengine waliopo sasa ambao mwaka 2005 walikuwa manaibu mawaziri ni Gaudencia Kabaka, Bernard Membe, Celina Kombani, Christopher Chiza na Mathias Chikawe.

Naibu waziri pekee ambaye alikuwamo katika baraza la mawaziri la kwanza la Rais Kikwete akiwa na wadhifa huohuo ni Dk Makongoro Mahanga ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira.

Waliotemwa
Mawaziri waliotemwa au kujiuzulu tangu Rais Kikwete aingie madarakani, wakiwamo wale walioshindwa katika kinyang’anyiro cha ubunge ni Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu, Antony Diallo, Dk Ibrahim Msabaha, Basil Mramba, John Chiligati, Andrew Chenge, Joseph Mungai, Dk Emmanuel Nchimbi, Lawrence Masha, Mustafa Mkulo, William Ngeleja, Dk Cyril Chami, Omary Nundu, Bakari Mwapachu na Kingunge Ngoimbale-Mwiru.

Wengine ni Ezekiel Maige, Dk Hadji Mponda, Teresa Huvisa, Shamsi Vuai Nahodha, Nazir Karamagi, Dk Mathayo David, Khamis Kagasheki, Profesa Anna Tibaijuka, Profesa Sospeter Muhongo, Dk Batilda Buriani, Joseph Mungai, Diodorus Kamala, Mohamed Seif Khatib, Mwantumu Mahiza, Profesa Peter Msola na Profesa David Mwakyusa, Philip Marmo na Juma Ngasongwa.

Naibu mawaziri ni Dk Luca Siyame, Balozi Seif Ally Idd, Hezekiah Chibulunje, Shamsa Mwangunga, Daniel Nsanzugwanko, Hezekiah Chibulunje, Rita Mlaki, Dk Charles Mlingwa, Zabein Mhita, Athuman Mfutakamba, Dk Lucy Nkya, Goodluck Ole Medeye, Benedict Ole Nangoro, Gregory Teu, Philipo Mulugo, Mohamed Abood, Dk Aisha Kigoda, Omari Yusuf Mzee, Jeremiah Sumari, Dk Maua Daftari, Zakia Meghji, Joel Bendera, Abdisalaam Issa Khatib na James Wanyancha.

Pia, wapo ambao walifariki dunia ambao ni Salome Mbatia, Juma Akukweti, Jeremiah Sumari na William Mgimwa.

Badiliko la Kwanza
Katika baraza lake la kwanza Rais Kikwete aliteua mawaziri na naibu mawaziri 60 Januari 2006 na ilipofika Oktoba 2006, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya kwanza makubwa ya baraza lake la mawaziri kwa kuwahamisha vituo vya kazi mawaziri 10 na naibu mawaziri wanane.

Mawaziri waliohusika na mabadiliko hayo ni Diallo (Maliasili na Utalii) ambaye alihamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Profesa Maghembe (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana) kupelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Dk Msabaha (Nishati na Madini) alihamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Karamagi (Viwanda na Biashara) alihamishiwa Wizara ya Nishati na Madini, Mramba (Miundombinu) alihamishiwa Viwanda na Biashara na Chiligati (Mambo ya Ndani) alihamishiwa Wizara Kazi, Ajira na Vijana.

Mawaziri wengine ni Chenge (Ushirikiano Afrika Mashariki) alihamishiwa Wizara ya Miundombinu, Dk Kawambwa (Maendeleo ya Mifugo) alihamishiwa Wizara ya Maji, Wasira (Maji) alihamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Mungai (Kilimo, Chakula na Ushirika) alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Naibu Mawaziri waliohamishwa wizara zao na kupelekwa wizara nyingine ni Dk Nchimbi (Habari, Vijana, Michezo na Utamaduni) kwenda Wizara ya Kazi, Nsanzugwanko (Kazi na Ajira) kwenda Wizara ya Habari, Michezo na Utamaduni, Dk Mathayo (Biashara na Viwanda) kwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Chibulunje (Kilimo, Chakula na Ushirika) kwenda Wizara ya Viwanda na Biashara.

Wengine ni Dk Buriani (Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto) kuhamishiwa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Mbatia (Mipango, Uchumi na Uwezeshaji) kwenda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Masha (Nishati na Madini) kwenda Mambo ya Ndani na Membe (Mambo ya Ndani) kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.

Badiliko la Pili
Februari 2007, Rais Kikwete alifanya uteuzi wa mawaziri wawili na naibu waziri wawili baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Asha-Rose Migiro kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Nafasi ya Migiro ilichukuliwa na Membe.

Dk Buriani aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge na Uratibu) kujaza nafasi iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Akukweti. Kabla ya uteuzi huo Buriani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwekezaji.

William Ngeleja aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na Gaudence Kayombo aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji.

Badiliko la tatu
Februari 12, 2008 baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond, Kikwete alivunja Baraza la Mawaziri na kuliunda upya.

Lowassa alijiuzulu sambamba na waliokuwa mawaziri wawili Dk Msabaha na Karamagi ambao wote walikuwa wameiongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti. Nafasi zao zilizibwa na William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Kamala (Afrika Mashariki), huku Pinda akiteuliwa kuchukua nafasi ya Lowassa.

Badiliko la nne
Rais Kikwete alifanya mabadiliko mara ya nne katika baraza lake Mei, 2008 baada ya Chenge, ambaye ni mbunge wa Bariadi, kujiuzulu kutokana na kashfa ya ununuzi wa rada na nafasi yake kujazwa na mbunge wa Bagamoyo, Dk Kawambwa huku Rais Kikwete pia akibadilisha mawaziri kadhaa.

Badiliko la tano
Mei 2012, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya tano katika baraza lake baada ya kuwaondoa mawaziri sita baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa walikiuka maadili ya utumishi wa umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.

Katika mabadiliko hayo waliondolewa walikuwa ni Mkulo (Fedha), Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Maige (Maliasili na Utalii), Nundu (Uchukuzi) na Dk Chami (Viwanda na Biashara). Wengine waliotemwa ni Mfutakamba (Naibu, Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Nkya.

Mawaziri walioziba nafasi hizo ni William Mgimwa (Fedha), Kagasheki (Utalii), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Dk Mwinyi (Afya), Profesa Muhongo (Nishati na Madini), Dk Seif Rashid (Naibu, Afya) na George Simbachawene (Naibu, Nishati na Madini).

Manaibu wapya walioingia ni January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo). Wengine ni Dk Binilith Mahenge (Maji), Stephen Masele (Nishati na Madini), Angela Kairuki (Katiba na Sheria), Janet Mbene na Saada Mkuya Salum (Fedha).


Badiliko la sita
Januari 19, 2014, Rais Kikwete alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuteua mawaziri wapya wawili na manaibu mawaziri wapya wanane, huku akiwapandisha vyeo manaibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliwapumzisha Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Wengine waliopumzishwa ni Benedict Ole-Nangoro aliyekuwa naibu waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye aliyekuwa naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mabadiliko hayo yalikuwa yanalenga kujaza nafasi zilizoachwa na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii, Dk Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk Mathayo (Maendeleo ya Mifugo) waliotemwa Desemba 2013 kutokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza na nafasi ya Dk Mgimwa, aliyefariki dunia kutokana na maradhi.

Mawaziri wapya walioteuliwa wakati huo ni Dk Asha-Rose Migiro (Katiba na Sheria), Dk Titus Kamani kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wengine aliowateua kuwa naibu mawaziri ni Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Kebwe Stephen, Naibu Waziri, Afya na Ustawi wa Jamii na Jenista Mhagama, naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Pia, Dk Pindi Chana aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Kaika Telele, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. 

Wengine ni Godfrey Zambi, naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika, Juma Nkamia, Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mahmoud Mgimwa, Naibu Waziri, Maliasili na Utalii.


Naibu mawaziri waliopandishwa kuwa mawaziri ni Saada Mkuya (Waziri wa Fedha), Lazaro Nyalandu (Maliasili na Utalii) na Dk Seif Seleman Rashidi ( Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Binilith Mahenge alipandishwa kutoka Naibu Waziri wa Maji na kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).

Dk Hussein Ali Mwinyi alihamishwa kutoka Afya na Ustawi wa Jamii kwenda Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na wengine kadhaa walihamishwa.


Badiliko la saba
Juzi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko ya saba ambayo yanawezekana kuwa yatakuwa ya mwisho kutokana na kusalia miezi sita kabla ya kuvunjwa kwa Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba.

Mabadiliko hayo baada ya mawaziri wawili, Profesa Tibaijuka (kufutwa kazi) na Profesa Sospeter kujiuzulu kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Tegeta Escrow.

Walioingia ni manaibu waziri wawili, Charles Mwijage (Nishati na Madini) na Anna Malecela (Elimu na Ufundi). 

Wengine walihamishwa ambao ni Wasira kutoka Ofisi ya Rais kwenye Kilimo na Ushirika, Lukuvi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wengine ni Dk Nagu kwenda Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) na Jenister Mhagama (Waziri Mkuu, Uhusiano, Uratibu na Bunge).

Dk Harrison Mwakyembe anahamia Afrika Mashariki (kutoka Uchukuzi) na nafasi yake inachukuliwa na Sitta akitokea Wizara ya Afrika Mashariki.

Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527