Makubwa haya!! MTENDAJI WA KATA AMWAPISHA MWENYEKITI BILA UCHAGUZI,KITONGOJI CHA IKIGIJO KIJIJI CHA KIKWETE

Mtendaji wa kata ya Kakubilo Zefania Chembe akiwa ofisini kwake-Picha na Valence Robert-Malunde1 blog Geita
Katika hali isiyokuwa  ya kawaida Mtendaji wa Kata ya Kakubilo Wilaya ya Geita Mkoani  Geita Zefania Chenge amemwapisha mwenyekiti wa kitongoji cha Ikigijo Kijiji cha Kikwete  Balele Ngulu wa (CCM), kuwa mwenyekiti wa kitongoji hicho.


Zefania alimwapisha mwenyekiti huyo ambaye hakuchaguliwa na wananchi kupitia kikao cha kamati tendaji ya kijiji cha Kikwete kilichofanyika Januari 23 mwaka huu.

Ngulu alisimikwa kuwa mwenyekiti wa kitongiji hicho baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Disemba 14 mwaka jana, kutokana na kucheleweshwa kwa fomu za wagombea wa uenyekiti kutoka CHADEMA na CCM na hivyo kutakiwa kusubiri baada ya siku 90 kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

Kufuatia hali hiyo Viongozi wa Kata ya Kakubilo (UKAWA)  waliiomba serikali itengue mara moja uamuzi huo vinginevyo wanaandaa maandamano yasiyokuwa na kikomo katika kata hiyo.

“Sisi kama viongozi wa Ukawa tunamuomba mkurugenzi atengue huu uamuzi wa kuapishwa kwa mwenyekiti huyu sisi pamoja na wananchi hatumtambui na tutaandamana kwa ajili ya hili”,alisema Abdallah Machimu ambaye ni katibu wa Ukawa kata ya Kakubilo.

Kwa upande wa wananchi  wa kitongoji hicho walimkataa mwenyekiti huyo na kudai kuwa wao hawamtambui.
 
“Mwenyekiti huyu aliyeapishwa na Mtendaji sisi hatumtaki kwa sababu hatukumchagua na wala uchaguzi haukufanyika katika kitongoji chetu, sasa huyu bwana wamemtoa wapi mbona tunafanyiwa mambo ya ajabu au kwa vile ni kijijini wanatufanya sisi wajinga? Tunasema hatumtaki,’’walisema wananchi hao.

Malunde1 blog  ilimtafuta mtendaji huyo kutaka kujua  tuhuma hizo ni za kweli ama ala, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokelewa na badaaye kuzimwa.

Hivi karibuni Chenge alituhumiwa na wananchi wa kijiji cha Kabayole kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za  mradi wa chumba kimoja cha Darasa katika shule ya msingi Kabayole baada ya kujenga darasa chini ya kiwango hivyo kulidanganya baraza la madiwani la mwaka 2014  kuwa boma limekamilika wakati ni uongo.

Hayo yalibainishwa na wananchi wa kata hiyo wakishirikiana na viongozi wa Chama pinzani (CHADEMA) baada ya kugundua jengo la darasa hilo halijakamilika na liko chini ya kiwango. 


Kufuatia taarifa iliyopelekwa katika baraza la madiwani ya Januari 2014 na mtendaji huyo juu ya kukamilika kwa mradi huo, ni ya uongo kwani jengo hilo lilikuwa bado halijakamilika mpaka sasa.



Uchunguzi uliofanywa kuhusiana na mradi huo umebainisha kuwa pesa nyingi kiasi cha Sh. Milioni 9 zimeorodheshwa ambazo ni gharama za mradi kutumika, ambapo kiuhalisia kiongozi huyo amejilipa mamilioni ya mradi huo, huku akilidanganya baraza la madiwani pamoja na wananchi.



Kutokana na hali hiyo wananchi wamepinga mradi huo na kumtaka mtendaji huyo arejeshe mara moja fedha hizo na wameiomba serikali imfute kazi mtendaji huyo.



“Jamani sisi tunashangaa tumechangishwa pesa, kwa kuuza kuku, bata, mbuzi pamoja na masufuria yetu…ili tuchangie chumba hiki cha darasa lakini kiko chini ya kiwango na halijakamilika sisi tulifikisha sh. Milioni tatu na serikali ilitoa sh. Milioni tisa kukamilisha mradi huo,”alisema Joshua Juma.



Vilevile wananchi hao waliendelea kumlalamikia mtendaji huyo , kwa kuwakamata kwa ajili ya kuchangia maabara jambo ambalo walisema limekuwa kero kwao .




“Jambo jingine amekuwa akitukamata tunapigwa na migambo wake na kubambikiziwa kesi kwa ajili ya maabara tunanyanyasika kweli hatuna imani na mtendaji huyu, tunaishi kwa mashaka ndani ya nchi yetu,”walisema wananchi hao.




Hata hivyo alipotafutwa na waandishi wa habari  Chenge aligeuka mbogo na kutaka kuigeuza ofisi kuwa uwanja wa masumbwi huku akiwatimua waandishi wa habari.



“Jamani sitaki kuwaona ,mmekuja kutafuta nini hapa nawaombeni mtoweke mara moja sina shida na nyinyi na sitaki ugomvi na nyinyi waandishi”alisema Chenge.


Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527