KUHUSU MATOKEO YA KIDATO CHA PILI 2014,WATAKAORUDIA NI 29,770

Baraza la Mitihani (Necta), limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili  ya mwaka 2014,  ambapo limesema ufaulu umepanda kwa asilimia 3.32 ikilinganishwa na mwaka juzi.

Matokeo hayo yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Dk. Charles Msonde, akisema tathmini ya awali ya matokeo ya jumla inaonyesha, ufaulu umepanda kwa asilimia 3.32 kutoka asilimia 89.34 mwaka juzi na kufikia asilimia 92.66 mwaka jana.

Hata hivyo, amesema kuwa ufaulu wa juu zaidi ni katika somo la Historia ambapo asilimia 90.71 ya watahiniwa somo hilo wamefaulu, wakati Hisabati limeshika mkia kwa asilimia 18.15.

 Dk. Msonde alisema jumla ya watahiniwa 453,191 waliandikishwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 233,834, sawa na asilimia 51.60 na wavulana ni  219,357 sawa na asilimia 48.40.

Alisema kati ya watahiniwa hao, waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 405,204 , sawa na asilimia 89.40 ambapo 47,987 sawa na asilimia 10.60 hawakufanya.

Alisema katika ufaulu wa jumla,  watahiniwa 375,434 (asilimia 92.66) ya waliofanya mtihani walipata alama zinazowawezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tatu. Kati yao wasichana ni 195,328 na wavulana ni 180,106.

WATAKAORUDIA
Dk. Msonde alisema watahiniwa 29,770 sawa na asilimia 7.34 wamepata alama ambazo baraza limeona ni vema wakarudia kidato cha pili ili waweze kumudu masomo kabla ya kuendelea kidato cha tatu.

Alisema mwaka 2013 kati ya watahiniwa 472,833 waliofanya mtihani huo, walioweza kupata alama za kuendelea na kidato cha tatu walikuwa ni 422,446 (asilimia 89.34).

“Matokeo ya sasa idadi ya wanafunzi waliopata madaraja mazuri ya ufaulu ni 180,965 (asilimia 44.66), watahiniwa wamefaulu vizuri zaidi katika masomo ya Historia, Kiswahili, Kiingereza na Uraia ambapo idadi yao ni zaidi ya asilimia 84.0 ya watahiniwa,” alisema na kuongeza:

“Watahiniwa wamefaulu vizuri katika masomo ya Jiografia, Biolojia na Utunzaji wa Mahesabu (Book Keeping) ambapo ufaulu upo kati ya asilimia 50 hadi 70,” alisema.

UFAULU WA CHINI
Dk. Msonde alitaja asilimia kwenye mabano ya masomo yaliyo chini ya asilimia 50 kuwa ni Hisabati  (18.15), Kilimo (34.45), Kemia (38.48), Fizikia (38.72) na Biashara (42.65).

Kutokana na hilo, katibu huyo amewashauri watafiti wa elimu kujikita kwenye utafiti wa masomo hayo ambayo hajayafanya vizuri kwa kutumia matokeo ya wanafunzi hao, kwenda shuleni kujua sababu ni nini.

“Ukiangalia majibu ya watahiniwa kwenye masomo hayo yanaonyesha wazi hawana uelewa wa kutosha maarifa na stadi zao hazijafikia sehemu nzuri, bado kuna tatizo kwenye masomo haya, lazima tujue tatizo ni walimu, mazingira au wanafunzi wenyewe,” alisema.

Alisema baadhi ya watahiniwa wameonyesha umahiri wa juu kwa kupata alama 100 ambapo katika somo la Kiingereza waliofanya vizuri ni  41, mahesabu ni tisa huku Biolojia, Uraia  na Utunzaji wa Mahesabu wametoka mmoja mmoja.

Katibu huyo ametoa wito kwa wadau wa elimu, kuhakikisha juhudi za makusudi zinafanyika kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ambayo hayakufanya vizuri unaimarishwa ili kuinua ufaulu kabla ya kuingia kidato cha nne.

Pia amewataka walimu na wanafunzi kuendeleza juhudi katika ufundishaji na ujifunzaji katika masomo yaliyofanya vizuri ili watoto waimarike zaidi.

“Maafisa elimu wa mikoa na wilaya, wakaguzi wa shule fuatilieni hili katika kuhakikisha maeneo yanayotakiwa kutiliwa mkazo hilo linafanyika, wazazi na walezi nanyi toeni ushirikiano kwa walimu ili kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni,” alisema.

Mtihani wa FTSEE ulianza rasmi kuendeshwa na baraza hilo kuanzia mwaka jana ambapo awali ulikuwa ukiendeshwa kila mwaka na Idara ya Ukaguzi wa Elimu kuanzia mwaka 1999 uliporejeshwa baada ya kusitishwa mwaka 1994.


Lengo la mitihani hii ni kutoa tathmini endelevu ya mwanafunzi kubaini maarifa, ujuzi, na mwelekeo aliokuwa nao baada ya kipindi cha miaka miwili ya elimu shule ya sekondari.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI 

Bonyeza hapa Tukupe habari zote mara moja zikitoka "HABARI" VITUKO "MAPENZI"MAGAZETI,UDAKU>
Endapo una Habari,Picha,Video,Tangazo au Tatizo Lolote wasiliana nasi kwa namba  +255 688 405 951

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527