ACT TANZANIA WAMILILIA MWENYEKITI WAO ALIYEUAWA KWA KUKATWA KICHWA NA NYETI ZAKE HUKO KATAVI


Chama cha ACT-Tanzania kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika na tukio la mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masigo wilayani Mlele mkoani Katavi, Christian Kahongo. 

 
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa ACT-Tanzania, Samson Mwigamba, ilieleza kuwa chama hicho kinalaani mauaji hayo ya kinyama ambayo hayaendani na haki za binadamu.
 
Alisema walimkata kichwa na kukitenganisha kabisa na kiwiliwili kisha wakakata sehemu za siri na baadhi ya viungo vingine vya kichwa wakaanza kuvikaanga kwenye sufuria.
 
Alisema huo ulikuwa ni unyama wa ajabu ambao hatujawahi kuushuhudia.
 
“ACT-Tanzania tumepoteza shujaa namba moja kati ya mashujaa wanaokiwakilisha chama chetu kwenye vyombo vya Serikali. Ndiye mshindi wa kwanza kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kupitia ACT-Tanzania na alipita bila kupingwa na kuwa wa kwanza kutangazwa kuwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Masigo kupitia ACT-Tanzania.
 
“Tumepoteza shujaa kama chama taifa, Mkoa wa Katavi umepoteza shujaa, Jimbo la Mlele wamepoteza shujaa, vivyo hivyo kwa wanachama wa Kata ya Inyonga na tawi la Inyonga,” alisema Mwigamba.
 
Alisema chama kitashiriki msiba huo kwa kuwakilishwa na Mwenyekiti Taifa wa muda pamoja na Katibu wa Ngome ya Vijana Taifa.
 
“Ikumbukwe kuwa wauaji hawana rangi, kabila wala vyama, pia hawachagui nani wa kumuua kama ilivyotokea hivi karibuni kwa askari wetu katika Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
 
“Sisi ACT-Tanzania tunalaani kwa nguvu zote mauaji haya ya kiongozi wetu si tu kwa sababu aliyeuawa ni kiongozi wa ACT-Tanzania, bali tutalaani na kupinga mauaji ya Mtanzania yeyote,” alisema Mwigamba.
 
Tukio hilo la mauaji ya kinyama lilitokea Januari 24, mwaka huu ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwa Christian Kahongo na kumuua kwa kumkatakata mapanga huku wakimtenganisha kichwa na kiwiliwili,sehemu za siri kisha kuweka kwenye sufuria na kuzipika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527