MAALIM SEIF ATEMBELEA ENEO LA JENGO LILILOANGUKA MJI MKONGWE ZANZIBAR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akimsikiliza Kamanda Ame Ali ambaye ni kiongozi wa shughuli za usafishaji wa eneo lilipoanguka jengo la ghorofa huko Shangani mjini Zanzibar.
 

Na Khamis Haji , OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amezitaka Mamlaka zinazosimamia majengo katika enelo la Mji Mkongwe Zanzibar kuwa na utaratibu mzuri wa kuyakagua ili kuhakikisha uimara wake na kuepusha maafa kwa watumiaji na jamii nzima.

Maalim Seif amesema hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za uondoaji kifusi katika jengo lililoanguka jana katika eneo la Shangani mjini Zanzibar, zoezi linalofanywa na askari wa Kikosi cha Zimamoto, Manispaa pamoja na wananchi wa Mji Mkongwe.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema nyumba zilizopo katika Mji Mkongwe zinasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya Mji Mkongwe au Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana, hivyo taasisi hizo ni jukumu lao kuzigagua uimara wake na kuhakikisha ni madhuti.

Amesema pale ambapo taasisi hizo zitabaini kuna nyumba ambazo zimechakaa zinazoweza kuanguka na kuhatarisha maisha ya watu na mali zao ni vyema kuwataka watumiaji wake wahame, ili kuepusha kuangukiwa na nyumba hizo na kuhatarisha maisha yao.
Katika ziara hiyo, ambapo alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis na Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Mhe. Ismail Jusa Ladhu alivipongeza vikosi vinavyoendesha shughuli za Uokoaji na wananchi wa Mji Mkongwe kwa kazi kubwa ya uokozi wanayoifanya.

Naye Mkuu wa Kituo cha Zimamoto na Uokozi Makao Makuu, Ame Ali ambaye anaongoza shughuli za uokozi na usafishaji wa eneo hilo amesema kazi hiyo inaendelea vizuri na walitarajia kuikamilisha leo.

Amesema jengo hilo lililoanguka jana asubuhi lilikuwa halikaliwi na watu kutokana nakukabiliwa na uchakavu na hakuna mtu aliyepoteza maisha au kujeruhiwa kufuatia tukio hilo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527