MWANAMME AUAWA KWA KUKATWA MAPANGA SHINYANGA AKILA CHAKULA USIKU


Mwanamme aitwaye Mageni Buhimili(54) mkazi wa kijiji na kata ya Mwakitolyo wilaya ya Shinyanga ameuawa kwa kukatwa panga kichwani,mikononi na tumboni wakati akila chakula cha usiku nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha amesema tukio hilo limetokea Oktoba 26 mwaka huu saa moja na nusu usiku.


Kamanda Kamugisha alisema mwanamme huyo mkazi wa kitongoji cha Mahiga kata ya Mwakitolyo akiwa anakula chakula cha usiku ghafla alivamiwa na watu wasiojulikana kisha kumuua kwa kumkata panga kichwani,mikononi na tumboni.


Alisema juhudi za kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo zinaendelea.


Wakati huo huo jeshi la polisi linawashikilia watu watatu wakazi wa kata ya Idahina wilayani Kahama kwa kosa la kukutwa wakimiliki silaha aina ya bastola na gobole kinyume cha sheria.

Kamanda Kamugisha alisema watu hao walikamatwa Oktoba 27 mwaka huu.


Aliwataja watu hao kuwa ni Magashi Magunga(21) mkazi wa Chato mkoa wa Geita na Masumbuko Juma(27) mkazi Ushirombo ambao walikamatwa kwa kupatikana na silaha aina ya bastola.


Alisema silaha hiyo imetengenezwa kienyeji isiyokuwa na namba za usajili wakimiliki kinyume cha sheria na kwamba wanahojiwa ili kubaini matukio ya kihalifu waliyokuwa wakiyafanya.


Alimtaja mtuhumiwa wa tatu kuwa ni mwanamke aitwaye Kashindye Mgaiwa(38) aliyekamatwa kwa kosa la kupatikana na silaha aina ya gobole lililotengenezwa kienyeji na halina namba.


Kamanda huyo aliongeza kuwa mtuhumiwa alikuwa akilimiliki bila kibali na inasadikiwa alikuwa akilitumia kutenda uhalifu.


Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527