TAARIFA RASMI KUHUSU AJALI YA BASI LA SUPER NAJIMUNISA LILILOPINDUKA BAADA YA TAIRI KUPASUKA LEO SHINYANGA

 Mmoja wa majeruhi katika ajali hiyo bwana Boniface Ntotole aliyekuwa anasafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam akiwa ndani ya wodi namba 5 katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga leo baada ya kutokea ajali

 Huduma kwa majeruhi zikiendelea ambapo imeelezwa kuwa majeruhi waliolazwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga ni 22,kati yao wanaume ni 13 na wanawake 9

Awali baada ya ajali
Basi la Supernajimunisa likiwa limeharibika vibaya baada ya kupata ajali leo Usanda-Samuye Shinyanga
Kaimu mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Shinyanga lnsp Vicent Msami akikagua ajari ambapo alisema ajari hiyo pia imechangiwa na mwendo kasi

Wataalamu wa wakiendelea kutoa huduma ya tiba kwa wahanga wa ajari ya basi la Najmunisa katika eneo la tukio
Vilio vilitawala,majeruhi wakiwa taabani baada ya kupata maumivu sehemu mbalimbali za mili yao na hapa wanapatiwa matibabu
Umati mkubwa wa watu wakiwa wamekusanyika kwenye ajari ya basi la Najmunisa 

Basi la supernajimunisa likiwa eneo la tukio leo abiria wakihangaika baada ya ajali hiyo ambayo imejeruhi watu 52 kati 63 waliokuwa ndani ya basi hilo
Abiria wakihangaika baada ya ajali

Basi likiwa limepinduka

Wimbi la ajali za barabarani limeendelea nchini ambapo leo abiria 63 waliokuwa wanafasafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es salaam na basi la Super najimunisa lenye namba za usajili T.242 BRJ wamenusurika kufa baada ya basi hilo kupinduka katika kijiji cha Busanda kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga mkoa wa Shinyanga leo majira ya saa tatu asubuhi.

Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina la Dickson Paulo 

Majeruhi 52 walikimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu.

Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt Ntuli Kapologwe ameiambia malunde1 blog kuwa wamepokea majeruhi 52 ambapo kati yao majeruhi waliolazwa ni 22 na miongoni mwa ambao wanne kati yao hali zao ni mbaya na tayari majeruhi 30 wamesharuhusiwa.

 Katika hatua nyingine malunde1 blog imezungumza na majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo ambao wamesema ajali hiyo imetokea baada ya tairi la mbele la basi hilo kupasuka na gari kupinduka mtaroni

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kwamba pamoja na kupasuka kwa tairi basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi.

Kamanda Kamugisha alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.

Hata hivyo eneo hilo la Usanda limekuwa sugu kwa matukio ya ajari za barabarani za mara kwa mara na kusababisha vifo vya watu na ulemavu wa kudumu

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog-Shinyanga 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527