WANAOPUUZA WAASISI WA TAIFA WANA KANSA YA UBONGO

Wananchi wa kijiji cha Mwamashimba kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamesikitishwa na vitendo vya baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba vya kutukana na kudhihaki waasisi wa taifa na kudai kuwa watu hao  wanaokashfu viongozi huenda wana ugonjwa wa kansa ya ubongo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho,wananchi hao walisema vitendo vya kuwakosea heshima waasisi wa taifa akiwemo baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Amani Abeid Karume siyo vya kiungwana kwani viongozi hao ndiyo waliolifikisha taifa hapa lilipo.

Walisema kumekuwa na tabia ambazo siyo za kiungwana tena kinyume na maadili ya kitanzania zinazofanywa na baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba kama vile kudhihaki kazi waliyofanya waasisi hao kuunganisha nchi mbili Tanganyika na Zanzibar.

Mmoja wa wananchi hao aliyejitambulisha kwa jina la Shija Manoni alisema waasisi hao walifanya kitu kizuri cha kuunganisha nchi mbili kutokana na upeo na ulewa wao na kwamba kama kuna mapungufu basi wangetumia ufahamu na elimu zao kutatua changamoto za muungano lakini siyo kuuvunja.

“Ndugu waandishi,unajua kwa mtu mwenye akili timamu kuwapuuza waasisi wa taifa, ni laana kubwa,waasisi hawa ndiyo waliosababisha tuishi kwa mshikamano,upendo na amani,na ndiyo walisababisha hata hawa wanaojiita wasomi kupata kupata elimu wanayayojivunia”,aliongeza Manoni.

Kwa upande wake bi Malimi John mkazi wa kijiji hicho mwenye umri wa miaka 68 aliyekuwa akiongea kwa shida kwa lugha ya kisukuma alisema watu wasiojua kusoma walidai uhuru na waasisi wa taifa,na baada ya kupata uhuru walijiwekea mikakati ya kusomesha watoto ili waje kuwa wataalamu kuisaidia nchi na matokeo yake wasomi hao wameanza kutukana wazee.

“Sisi tunashangaa kusikia wasomi wetu wanadharau waasisi wa taifa hadi baba wa taifa,wakati sisi tunamweshimu alitutoa mikononi mwa wakoloni,tukawa kitu kimoja,hivi hawa wana akili timamu kweli,au wana matatizo ya kansa ya ubongo?”,alihoji mama huyo.

Bi John alisema ni vyema wajumbe wa bunge la katiba wakatumia elimu yao kutatua changamoto za muungano badala ya kuanzisha ujanja ujanja wa kuvunja muungano kwani muungano ndiyo umelifikisha taifa hapa lilipo.

via>>Zanzibar Leo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments