UMOJA WA MATAIFA WATUA SHINYANGA-FUATILIA HAPA ZIARA YA MAAFISA WA UN LEO SHINYANGA,WAKUTANA NA WANAFUNZI SHULE 10 ZA SEKONDARI,VYUO NA WALIMU, DC SHINYANGA AHUDHURIA WARSHA



Aliyesimama ni afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania (UNIC)bi Usia Nkhoma Ledama akizungumza leo katika katika viwanja vya Mazingira senta mjini Shinyanga kwenye warsha ya siku moja iliyokutanisha shule 10 za sekondari,vyuo na walimu kutoka katika shule na vyuo hivyo vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga, ambapo alisema umoja wa Mataifa(UN) unalipa suala la elimu kipaumbele sana kwa wanafunzi hivyo kuwataka wanafunzi kuwa na malengo katika maisha yao kwa kusoma kwa bidii,kuepuka vishawishi vinavyopelekea kupata ujauzito wakiwa wanafunzi tena chini ya umri wa miaka 18.Afisa habari huyo pia akatumia fursa hiyo kuwatahadhalisha wanafunzi wa kike  kuepuka ngono kwani kwa mujibu wa utafiti wao takwimu zinaonesha kuwa vijana wa kike wenye umri wa miaka 15-19 wana uhusiano wa kingono na wanamme wanaowazidi miaka juu zaidi ya umri wao hivyo kuwepo kwa hatari ya kuambukizwa VVU na mimba za utotoni.Kushoto ni
Mwenyekiti wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA) tawi la Shinyanga bwana Ezra Manjerenga

Wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari  kama vile Busurwa,Uhuru,Mazinge,Buluba,Chamaguha,Kizumbi, wakimsikiliza
Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania bi Usia Nkhoma Ledama ambaye alisema kwa mujibu wa sensa yao mwaka 2012 asilimia 65 ya Watanzania wote vijana wenye umri wa miaka chini ya 24,lakini pia asilimia 40 ya vijana wa kike wenye miaka chini ya 18 wanapata mimba za utotoni na wengine kuolewa katika umri huo.Aliongeza kuwa asilimia 23 ya vijana umri wa miaka 15-19 wameanza kuzaa na katika umri huo kati ya vijana wanne basi mmoja anaolewa ama kupata mimba

Wanafunzi wa vyuo vya VETA,MUCCOBS,Shycom , wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari  kama vile Busurwa,Uhuru,Mazinge,Buluba,Chamaguha,Kizumbi,waliohudhuria katika warsha hiyo ya Umoja wa Mataifa wakimskiliza Afisa habari kutoka UN,ambaye aliwataka  kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Umoja wa mataifa hapa nchini,lakini pia kuwaomba wazazi na walezi wa wanafunzi kujenga tabia ya kufuatilia mienendo ya watoto wao na kuwasaidia ili kuwafanya wapende elimu ili kufikia malengo ya millenia

 Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania bi Usia Nkhoma Ledama alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 52 ya vijana wa kike umri wa miaka 18-14 wameanza kufanya ngono na na asilimia 7 kwa wenye miaka 15-19 wanafanya ngono na wanamme wanaowazidi umri miaka 10 zaidi,huku vijana wa kiume wakidaiwa kuanza kufanya ngono wakiwa na umri wa miaka 20,akatumia fursa hiyo kuwataka vijana kuepuka ngono kwani wakindekeza ngono UKIMWI upo na hawataweza kutimiza ndoto zao hivyo.Alisema Umoja wa Mataifa haupo tayari kuendelea kuona vijana hawatimizi malengo yao



Aliyesimama ni bwana Innocent  Mkota mjumbe wa asasi ya vijana ya Umoja wa Mataifa Tanzania akizungumzia kuhusu klabu za Umoja wa Mataifa katika shule za sekondari na vyuoni ambapo alisema miongoni mwa faida ukiwa mwanachama wa klabu hizo ni kupata taarifa nyingi tena kwa wakati kutoka UN(kuwa karibu na umoja wa mataifa),kuhudhuria mikutano ya UN,kupata nafasi ya kusaidia jamii lakini pia kuwajengea uwezo wa aina mbalimbali kama vile kuongea mbele za watu,kuandaa ripoti,kupata vyeti n.k


Walimu na wanafunzi waliohudhuria warsha hiyo wakifuatilia kilichokuwa kinajiri katika eneo la viwanja vya Mazingira Senta mjini Shinyanga ambapo maafisa kutoka umoja wa mataifa walieleza kazi za umoja wa mataifa na wakatumia muda fursa hiyo kuitaka jamii kubadilika na kuhamasisha jamii kufuata uzazi wa mpango ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kupiga vita suala la vifo vya akina mama wajawazito na watoto,mimba za utotoni ambapo watoto wa kike milioni 7.5 miaka chini ya 18 wanazaa kila mwaka


Aliyesimama ni bwana Moses Mongo ambaye ni Mratibu wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kanda ya ziwa (UNA) akizungumza katika warsha eneo la Mazingira Senta mjini Shinyanga ambapo alisema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 1964 kote duniani na ndiyo taasisi pekee hapa nchini yenye klabu nyingi yenye lengo la kuwaunganisha watu wa chini na umoja wa mataifa.Alisema hivi karibuni wamefungua tawi la taasisi hiyo mkoani Shinyanga na mwenyeki wake ni bwana Ezra Manjerenga.Moses Mongo alitumia fursa hiyo pia kuwataka wanafunzi na wanajamii kwa ujumla kubadilika na kwamba mabadiliko yanaanza kwa kutenda na wafanye kazi kwa malengo ili kuleta mabadiliko katika jamii


Aliyesimama ni afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania bi Usia Nkhoma Ledama akizungumza jioni ya leo katika eneo la Mazingira Senta mjini Shinyanga katika warsha iliyokutanisha shule za sekondari kumi za manispaa ya Shinyanga lakini pia vyuo mbalimbali kama vile Chuo cha Ualimu cha Shinyanga,VETA na Chuo cha Ushirika(MUCCOBS),ambapo alieleza kazi mbalimbali za zinazofanywa na umoja wa mataifa hususani malengo ya millenia kama vile kuhamasisha afya ya uzazi,haki za binadamu,kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,umaskini,kuhamasisha amani na chakula kwa wenye njaa.Kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Anna rose Nyamubi ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Aliyesimama ni Mwenyekiti wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UNA) tawi la Shinyanga bwana Ezra Manjerenga akimkaribisha mkuu wa wilaya ya Shinyanga ndugu Annarose Nyamubi katika warsha hiyo iliyokutanisha shule 10 za sekondari na vyuo vitatu vilivyopo katika manispaa ya Shinyanga,katikati ni bi Harriet Macha,ambaye ni mkutubi kutoka kitengo cha habari Umoja wa Mataifa nchini Tanzania,wa kwanza kushoto ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna rose Nyamubi


Mgeni rasmi katika warsha hiyo,mkuu wa wilaya ya Shinyanga Anna rose Nyamubi,ambaye ni mdau wa maendeleo na mwanafamilia wa Umoja wa Mataifa(siku za nyuma aliwahi kufanya kazi na Umoja wa mataifa katika shirika la UNICEF),alisema nchi ya Tanzania inatekeleza malengo ya millenia kupitia  ilani ya ccm katika kuwaletea maendeleo wananchi wake hususani katika kupunguza umaskini.Katika hatua nyingine Nyamubi aliwataka vijana kuchangamkia fursa zinazotolewa na Umoja wa mataifa.Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa serikali inawajali vijana hivyo kuwataka kusoma kwa malengo kwani bila elimu dunia itawaacha na kuwataka kuacha kutegemea wazazi wao kwamba watarithi mali.Aidha Nyamubi alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi ambao hawajapeleka watoto wao kidato cha kwanza wawapeke haraka kabla ya kuwachukulia hatua.
Mapema leo kabla ya warsha-Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa nchini Tanzania bi Usia Nkhoma Ledama akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Chamaguha ambapo alisema lengo la ziara yao ni kuhamasisha  uanzishwaji wa klabu za Umoja wa Mataifa na kutoa elimu kuhusu shughuli za umoja wa mataifa ambapo huwa wanatembelea shule za msingi,sekondari na vyuo mbalimbali kuwaelimisha kuhusu ajenda za umoja wa mataifa kama vile changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, umaskini,ajira,afya ya uzazi,UKIMWI,mimba za utotoni,elimu n.k.
Aliyesimama ni bwana Moses Mongo ambaye ni Mratibu wa taasisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania kanda ya ziwa (UNA) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Chamaguha iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga,ambapo alisema shuke hiyo ni miongoni mwa shule chache zilizopata bahati kutembelea na Umoja wa mataifa na kuwataja miongoni mwa watu ambao ni mazao ya klabu za Umoja wa Mataifa kuwa ni Zitto Kabwe na John Mnyika.Alisema klabu za Umoja wa Mataifa zinawajengea wanachama wake ujasiri pamoja na kuwafundisha mambo mbalimbali kama vile elimu ya ujasiriamali


 Wanafunzi wa Shule ya sekondari Chamaguha wakinyoosha mikono kwamba wako tayari kuwa na klabu ya Umoja wa mataifa katika shule yao baada ya kuridhishwa na maelezo kutoka Umoja wa Mataifa hapa nchini wakiongozwa na Afisa habari kitengo cha habari Umoja wa mataifa Tanzania bi Usia Nkhoma Ledama

Awali katika shule ya sekondari Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga,ambako maafisa wa Umoja wa Mataifa walifanya ziara yao, Mkutubi kutoka kitengo cha habari Umoja wa Mataifa nchini Tanzania bi Harriet Macha akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo ambao wamedhamiria kuanzisha klabu ya Umoja wa Mataifa katika shule hiyo ambayo itaundwa na wanafunzi kuanzia 10 na kuendelea.Hapo anaonesha vitabu na vipeperushi mbalimbali vinavyohusu umoja wa mataifa ambao ulianzishwa mwaka 1945 baada ya vita ya pili ya dunia.Hivi sasa umoja wa mataifa una nchi wanachama 193 duniani kote na nchi 3 pekee siyo nchi wanachama wa Umoja huo,nchi hizo ni Taiwan,Cossovo na Vatican

Ni katika ofisi ya walimu katika shule ya sekondari Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga,muda mchache tu baada ya maafisa kutoka Umoja wa mataifa kuwasili katika shule hiyo kabla ya kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo.Aliyesimama ni kaimu mkuu wa shule hiyo bwana Malongo Maganga akiwakaribisha wageni hao ambapo aliupongeza Umoja wa Mataifa kwa kuwafikia na kufurahishwa na mpango wake kuhusu elimu ya uzazi wa mpango kwa wanafunzi kwani itawasaidia kuongeza uelewa na kujilinda zaidi ili kutimiza malengo yao.Alisema jamii inaamini kuwa elimu hiyo ni kwa ajili ya akina mama pekee.Aidha mwalimu Maganga alisema tayari shule yake imefungua faili kwa ajili ya klabu ya Umoja wa Mataifa kwa wanafunzi wa shule hiyo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments